Tume huru ya taifa ya uchaguzi imetangaza mabadiliko ya majina ya majimbo ya uchaguzi pamoja kuyagawa baadhi ya majimbo ili kupata majimbo mengine mapya manane kwa mujibu katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kanuni za tume huru ya uchaguzi.
Mabadiliko haya yanakuja Baada ya kupokea maombi kwa kuzingatia kanuni ya 18 (5) ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024, Tume ilitembelea na kufanya vikao na wadau katika baadhi ya majimbo yaliyoomba kugawanywa pamoja na majimbo yote.
Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma mwenyekiti wa Tume huru ya uchaguzi Jaji Jacobs Mwambegele, leo Mei 12, 2024 amesema Tanzania itakuwa na majimbo 272 ya uchaguzi pamoja na kata 3960 ikiwa tayari mabadiliko ya majina yamefanyika pamoja na majimbo mapya ya uchaguzi kuanzishwa.
"Kwa kuzingatia vigezo vya idadi ya watu, ambapo kwa majimbo ya mjini kigezo kilikuwa kuanzia watu 600,000 na kwa majimbo ya vijijini ilikuwa kuanzia watu 400,000, na masharti ya ibara ya 75(1), (2) na (4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ikisomwa pamoja na kanuni ya 18(7) ya Kanuni za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi za Mwaka 2024, baada ya kuchakata maombi husika, Tume imekubali na kuanzisha majimbo mapya nane (08)." Amesema Jaji Mwambegele.
Majimbo ya uchaguzi yaliyoanzishwa ni jimbo la Kivule na Chamazi mkoa wa Dar es Salaam, Jimbo la Mtumba mkoa wa dodoma, jimbo la Uyole mkoa wa Mbeya, jimbo la Bariadi Mjini mkoa wa Simiyu, majimbo ya Katoro na Chato kusini mkoa wa Geita na jimbo la Itwangi mkoa wa Shinyanga.
Majimbo yaliyobadiliswa majina ni pamoja na jimbo la Chato ambalo litakuwa jimbo la Chato kaskazini, jimbo la Nkenge kuwa Missenyi, jimbo la mpanda vijijini kuwa Tanganyika, Jimbo la Buyugu kuwa Kakonko, jimbo la Bariadi kuwa Bariadi vijijini na jimbo la Handeni vijijini kuwa jimbo la Handeni.
Aidha ameeleza kuwa majimbo matano ya mkoa wa Singida yamebadili majina ambapo jimbo la Manyoni mashariki litakuwa jimbo la Manyoni, jimbo la Singida kaskazini kuwa Ilongelo, Manyoni magharibi kuwa Itigi, Singida mashariki kuwa Ikungi mashariki, Jimbo la Singida magharibi kuwa Ikungi magharibi na mkoa wa tabora jimbo la Tabora kaskazini kuwa jimbo la Uyui.
Mabadiliko haya yamefanyika kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 ikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 10(1)(d) cha Sheria, ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imepewa mamlaka na jukumu la kuchunguza, kupitia mipaka na kugawa majimbo ya uchaguzi katika Jamhuri ya Muungano.
Mwisho.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved