Pichani:Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mh.Mwanamvua Mrindoko alipozungumza na Waandishi wa Habari(Hawapo pichani)Ofisini kwake 13 Mei 2022
Na:John Mganga-IO Katavi RS.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mh.Mwanamvua Hozza Mrindoko ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa Sekta ya Misitu na Nyuki pamoja na Wananchi Mkoani Katavi Kushiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani kuanzia tarehe 19 hadi 21 Mwezi Mei Mwaka 2022.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake 13 Mei 2022, Mh.Mrindoko amesema Mkoa wa Katavi umepewa heshima kubwa ya kuwa Mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani Kitaifa ambapo Mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii,Ofisi ya Rais TAMISEMI,pamoja na Wadau mbalimbali wapo katika maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Ufugaji Nyuki Duniani Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika katika Uwanja wa Azimio uliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda na kupambwa na Kaulimbiu inayosema Nyuki ni Uchumi,Tuwalinde na Kuhifadhi Mazingira yao”.
Ameeleza kuwa Maadhimisho haya Kitaifa yanafanyika Katavi kutokana na mchango wa sekta ya nyuki katika kukuza uchumi wa mkoa na wananchi kwa ujumla na kwamba mdudu nyuki amekuwa na mchango mkubwa katika uchavushaji wa mimea hali inayopelekea Mkoa wa Katavi kuendelea kubaki miongoni mwa mikoa inayojitosheleza kwenye chakula sambamba nakuzalisha chakula cha ziada kwa mikoa mingine.
Mh.Mrindoko amesema Lengo Kuu la maadhimisho hayo ni kuwaleta pamoja wataalam wa Nyuki, wafugaji wa Nyuki, wajasiriamali wa mazao ya Nyuki na wadau mbalimbali wa Nyuki kwa lengo la kujengeana uwezo wa namna bora ya kuendeleza Sekta ya Nyuki katika mkoa wa Katavi, Mikoa ya Kanda ya Magharibi na Nchini kwa ujumla.
Akizungumza kuhusu hali ya uzalishaji wa Mazao yatokanayo na Nyuki pamoja na faida zake Mh.Mrindoko amesema Katika kipindi cha miaka mitano (2016-2021) Mkoa wa Katavi umeshuhudia Sekta ya Ufugaji Nyuki ikiingiza kiasi cha Tsh. 13,440,900,000/= na Tsh. 4,047,984,500/= zilizotokana na lita 2,688,180 za asali na kilo 578,284 za Nta mtawalia.
Amesema Katika kipindi hicho, Mkoa pia umeshuhudia ongezeko la takwimu za ufugaji Nyuki katika nyanja tofauti, ambapo uzalishaji wa asali umeongezeka kutoka lita 387,431 mwaka 2016 mpaka lita 496,229 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 28. Uzalishaji wa Nta nao pia umeongezeka kutoka kilo 100,086 mwaka 2016 mpaka kilo 119,009 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 19.
Ratiba ya Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani inatarajia kuanza tarehe 19 - 21/05/2022 wageni watapata fursa ya Kubadilishana mawazo juu ya uboreshaji wa sekta ya Nyuki na pia watapata nafasi ya kujenga uelewa wa umuhimu wa Sekta ya Nyuki kupitia kongamano ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa. Miongoni mwa mada hizo ni ‘‘Athari za Mabadiliko ya tabia nchi kwenye shughuli za ufugaji nyuki’’ na ‘‘Fursa ya utalii wa nyuki na mchango wake katika uchumi’’
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved