Katibu Tawala Mkoa wa Katavi Bw.Hassan Abas Rugwa amewaasa watumishi Wilayani Tanganyika kudumisha ushirikiano na mahusiano mema kazini ili kufikia malengo mahsusi ya Serikali ya utoaji huduma bora kwa Wananchi.
Katibu Tawala Rugwa ametoa rai hiyo alipozungumza na Watumishi wa Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Tanganyika katika ziara yake Wilayani humo Septemba 5, 2022 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika,ikiwa ni sehemu ya ratiba yake kukutana na kuzungumza na watumishi wa kada mbalimbali Mkoani Katavi kwa lengo la kujitambulisha ikiwa ni muda mchache tangu kuwasili Katavi akitokea Kituo chake cha awali Dar Es Salaam.
Bw.Rugwa amewaambia watumishi wa Tanganyika kuwa kutokana na Watumishi wa Umma kutumia muda mwingi mahala pa kazi kuliko maeneo mengine ni muhimu kudumisha mahusiano mazuri kazini kwa kupendana na kuthaminiana ili kuboresha mazingira ya kazi jambo ambalo litasaidia kwa sehemu kubwa kufikia malengo mahsusi ya Serikali ya utoaji wa huduma bora kwa Wananchi.
Katibu Tawala Rugwa ameahidi ushirikiano wa kutosha kwa watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika akiwataka kutosita kufika ofisini kwake iwapo kuna changamoto yoyote ya kiutumishi inayowakabili watumishi hao.
Aidha Bw.Rugwa ameongeza kuwa ni furaha yake kuona watumishi wa Umma Mkoani humo wanapiga hatua kimaendeleo na kufikia malengo yao jambo ambalo linaleta Afya katika utumishi wa Umma.
“Kwa hiyo mimi matarajio yangu ni kuwa licha ya kuwa kiongozi naahidi kuwa mlezi mzuri wa watumishi,Katavi ni sehemu nzuri sana ya Watumishi kufikia matarajio yao”
Katibu Twala Rugwa pia ameongeza kuwa Mkoa wa Katavi ni moja kati ya mikoa Nchini inayokua kwa kasi zaidi ukilinganisha na mikoa mingine iliyoanzishwa miaka ya karibuni hivyo ni vema Watumishi wakatizama fursa za kuchumi zilizopo na kuzitumia ili kufikia malengo mahsusi ya kujiletea maendeleo.
Kwa Upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika Bw.Betuely Ruhega ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika licha ya mafanikio makubwa iliyoyapata bado inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa watumishi pamoja na Vitendea kazi ambapo amemuahidi Katibu Tawala Mkoa kuwa wanaendelea na jitihada za kutatua changamoto hizo.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved