Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amesema serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa wawekezaji mkoani Katavi kwa kufanya uwekezaji kuwa na manufaa kwa pande zote yaani muwekezaji, jamii na serikali.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa kikao kazi baina ya wawekezaji wa kampuni ya Katavi Mining company na ofisi ya Mkuu wa Mkoa leo Mei 21, 2025 kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Katavi ambapo amesema mkoa huu unafursa nyingi za uwekezaji ambazo bado hazijaanza kufanyiwa kazi.
"Tunawakaribisha sana wawekezaji katika sekta mbalimbali tumejiandaa kuhakikisha kuwa wanapata ushirikiano pamoja kuboreshewa mazingira na miundominu ya uwekezaji sawa na uhitaji wao ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi na kufikia malengo," amesema Mhe. Mrindoko.
Kikao hiki kililenga kuiwezesha kampuni ya uchimbaji wa madini ya Katavi Mining company Ltd, kuwasilisha na kuzungumzia dhumuni lake la kupanua uwekezaji katika sekta ya madini pamoja na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili ili waweze kuongeza uzalishaji.
"Changamoto iliyopo ni gharama kubwa ya uendeshaji wa shughuli zetu unaosababishwa na kukosekana kwa umeme ambapo chanzo chetu cha nishati kimekuwa kikitumia mafuta ambapo faida kubwa inaenda kwenye uendeshaji zaidi," amesema Mhandisi Abdallah Kipara.
Taarifa ya Afisa madini mkoa wa Katavi Mhandisi Andrew Mwalugaja amesema kuna eneo Kubwa la Uwekezaji Katika sekta ya Madini hasa madini ya Dhahabu na kopa kwani ni 20% pekee ya eneo lenye madini limeanza kuchimbwa katika mkoa wa katavi na tayari leseni za kati 15 zimetolewa kwa wachimbani na leseni nne pekee ndizo zinazofanya kazi huku leseni 3 zikiwa ni kutoka Katavi Mining company Ltd.
Akitoa hali ya upatikanaji wa umeme mkoani hapa Afisa masoko wa Tanesco Proches Joseph amesema serikali tayari imejenga Kituo cha Kupozea umeme katika eneo la Mpanda chenye msongo wa umeme wa Kv 33 kitaenda kumaliza kero ya kukosekana kwa umeme na kupunguza gharama ya uzalishaji viwandani na hata katika maeneo ya uchimbaji wa madini na unatarajiwa kuwashwa ifikapo June 2025.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved