Katavi, Machi 26, 2025
Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Florence Chrisant, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa watendaji wa Serikali katika kuhakikisha mafanikio ya programu ya usalama wa mtoto mtandaoni.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo kuhusu usalama wa mtoto mtandaoni, Bw. Chrisant amesema kuwa licha ya Serikali kuanzisha programu mbalimbali za kusaidia wananchi, changamoto ya ukosefu wa ushirikiano imeathiri utekelezaji wake.
“Kila mmoja anapaswa kuwajibika kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya madhara ya mitandao ya kijamii,” amesema Bw. Chrisant huku akiongeza kuwa matumizi mabaya ya mtandao yamechangia mmomonyoko wa maadili kwa watoto na vijana.
Amehimiza wazazi kuwa karibu na watoto wao, kuwapa mwongozo sahihi katika matumizi ya teknolojia, na kuhakikisha wanatumia mitandao kwa malengo chanya.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Usalama Mtandaoni, Bw. Yusuph Kileo, amesema tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 87 ya mitandao ya kijamii inachangia mmomonyoko wa maadili. Amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua za kulinda watoto dhidi ya ukatili wa mtandaoni kupitia programu hiyo.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Bi. Mwelinde Katto, amesema kampeni hii inalenga kutoa elimu kwa watoto, wazazi, walimu, na jamii kwa ujumla kuhusu usalama wa mtoto mtandaoni. Ameeleza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa asilimia 67 ya watoto wenye umri wa miaka 12 hadi 17 wanatumia mitandao ya kijamii, huku asilimia 5 wakilazimishwa kutuma picha zisizofaa.
Mafunzo hayo yamewaleta pamoja wataalamu wa Maendeleo ya Jamii, Maafisa Ustawi wa Jamii, Wakuu wa Dawati la Jinsia la Polisi, na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka mikoa ya Katavi, Rukwa, na Tabora.
Akihitimisha, Bw. Chrisant ameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa kuanzisha programu hiyo, akitoa wito kwa wadau wote kushiriki kikamilifu katika kulinda watoto dhidi ya hatari za mtandaoni.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved