WALENGWA WA MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASKINI WATAKIWA KUZINGATIA MASUALA YA LISHE
Bi.Asnath Mrema Afisa Lishe Mkoa wa Katavi akiongea na walengwa wa Mpango wa TASAF Mkoa wa Katavi amesema kuwa Mkoa wa Katavi bado haufanyi vizuri sana katika suala zima la lishe, hali ambayo inachangia kuwa na athari nyingi zinazotokana na hali ya lishe moja kwa moja au zinazochangia kuwepo na matatizo mengine ya kiafya kwa jamii ya wanakatavi kwa ujumla wake.
Bi.Asnath amesema kuwa pamoja na kuwa Mkoa wa Katavi ni miongoni mwa Mikoa inayozalisha chakula kwa wingi bado Mkoa unakabiliwa na tatizo kubwa la lishe kwa wananchi wake. Lishe duni ni moja ya matatizo makubwa ya kiafya yanayoathiri haswa watoto wadogo, wachanga na wanawake walio katika umri wa kuzaa nchini. Kwa watoto chini ya miaka 5 tafiti zinaonyesha kuwa hali ya udumavu katika Mkoa wa Katavi ni asilimia 39 ukilinganisha na asilimia 34 kitaifa. Uzito pungufu ni asilimia 15.4 kwa Mkoa wa Katavi na kitaifa ni asilimia 14.0. Upungufu wa damu ni asilimia 54.9 kimkoa na Kitaifa ni asilimia 57. Bi.Asnath amesema kuwa moja ya changamoto inayowakabili wanawake wenye umri wa miaka 15 – 49 ni upungufu wa damu ambapo kati ya wanawake kumi (10) watano (5) wanaupungufu wa damu.
Bi.Asnath amewaeleza walengwa hao kuwa pamoja na changamoto hizo Mkoa wa Katavi umejiwekea mikakati mingi ikiwemo, Kuhakikisha shughuli za lishe zimepangwa katika mipango ya idara mbalimbali ambazo zinahusika na masuala ya lishe kama Afya, Elimu, Kilimo, maendeleo ya jamii na maji. Kuendelea kutoa chanjo kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 5 na matone ya vitamin ‘A’ na dawa za minyoo kwa akinamama wajawazito na watoto chini ya miaka 5. Kuhimiza kila mkazi wa eneo la halmashauri mwenye uwezo wa kufanya kazi kuwa na shamba kwa ajili ya kuzalisha mazao ya chakula, mazao ya biashara, mbogamboga na matunda kwa ajili ya kupunguza tatizo la upungufu wa chakula na umasikini wa kipato ngazi ya kaya. Kuhusu suala la usalama wa chakula Bi.Asnath amesema kuwa imezuka tabia ya wakulima kuuza mazao yao yakiwa shambani, hii ni hatari na jambo ambalo linatakiwa kukemewa kwa nguvu zote na kuwataka walengwa waliopo katika Mpango wa TASAF kuhakiksha kuwa wanahifadhi chakula.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved