Kwa kutambua mchango mkubwa wa nyuki katika uchumi wa jamii na utunzaji wa mazingira, Mradi wa BEVAC unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia shirika lisilo la kiserikali la Enabel, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi, umeendesha ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo.
Ziara hiyo iliyoongozwa na Mratibu wa Mradi, Bi. Flosia Vugo, imelenga kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo cha kisasa cha usindikaji wa mazao ya nyuki pamoja na kujionea jinsi wanachama wa Chama cha Ushirika cha Mazao ya Nyuki wanavyoendelea kuongeza thamani ya mazao yao kupitia mbinu bora na zenye tija.
Akizungumza katika ziara hiyo, Katibu wa chama, Bw. Peter Kalula, alieleza kuwa chama hicho kilianzishwa mwaka 2022 kikiwa na wanachama 80, lakini hadi Julai 2025, idadi hiyo imeongezeka hadi kufikia wanachama 170, wakiwemo wanaume 140 na wanawake 30. Ukuaji huo wa haraka ni kielelezo cha mwitikio chanya kutoka kwa jamii na uhalisia wa fursa zilizopo katika sekta ya nyuki.
Hata hivyo, Bw. Kalula alitaja changamoto zinazokikabili chama hicho, ikiwemo umbali wa ofisi za utoaji vibali, kupanda kwa gharama za vibali katika kipindi kifupi, na ukosefu wa masoko ya uhakika kwa mazao yao. Alitoa rai kwa Serikali na Mradi wa BEVAC kusaidia upatikanaji wa mikopo kupitia taasisi za kifedha na kuwezesha ufunguzi wa masoko ya kudumu kwa bidhaa za nyuki.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia Uchumi na Uzalishalishaji Mkoa wa Katavi, Bw. Kayumba Torokoko, aliwapongeza wanachama kwa usimamizi madhubuti wa ujenzi wa kituo hicho na akawahimiza kuendelea na ubunifu, ikiwa ni pamoja na kuanzisha vyanzo mbadala vya mapato ili kuimarisha shughuli zao za ufugaji nyuki.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Bi. Christina Bunini, alikabidhi mizinga kwa wanachama wa chama hicho kama sehemu ya kusaidia jitihada za kuongeza uzalishaji, hatua inayoendana moja kwa moja na dhamira ya Mradi wa BEVAC ya kuimarisha miundombinu ya sekta ya nyuki na kuwawezesha wanavikundi kwa vitendea kazi muhimu.
Mpanda-Katavi (Mkoani Area)
Sanduku la Barua: Box 235, Mpanda -Katavi
simu: 025-2957108
Mobile:
Barua pepe: ras.katavi@tamisemi.go.tz
Copyright@2017 Katavi Rs. All right reserved